''People are being transformed into Jesus Christ through faith and the word of God''

Sunday, June 23, 2019

UMUHIMU WA NENO LA MUNGU

Mhubiri: Dr. Elifuraha Mumghamba
Maandiko: Mathayo 3:13-17, 4:1-11, Kutoka 8:2-3

Mstari wa kukumbuka
Mathayo 4:3-4 "Mjaribu akamjia akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, amuru kwamba mawe haya yawe mikate. Naye akajibu akasema, Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu."

Mtu hataishi kwa mkate tu, maisha yako hayapo katika vitu ya kushikika bali yapo katika kila Neno litokalo katika kinywa cha Mungu. Yesu alisema hayo baada ya kujaribiwa na shetani alipokuwa katika mfungo wa siku 40.

Uhai wako uko katika Neno la Mungu, uhai wako hauko katika chakula pekee. Neno la Mungu ni la muhimu sana kwako. Uhai wetu uko katika Yesu mwenyewe.

1Wakorintho 10:1-6 "Kwa maana, ndugu zangu, sipendi mkose kufahamu ya kuwa baba zetu walikuwa wote chini ya wingu; wote wakapita kati ya bahari; 2 wote wakabatizwa wawe wa Musa katika wingu na katika bahari; 3 wote wakala chakula kile kile cha roho; 4 wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni Kristo. 5 Lakini wengi sana katika wao, Mungu hakupendezwa nao; maana waliangamizwa jangwani. 6 Basi mambo hayo yalikuwa mifano kwetu, kusudi sisi tusiwe watu wa kutamani mabaya, kama wale nao walivyotamani."

Wana wa Israel walikula mana njiani lakini walifia njiani, kwasababu walimkasirisha Mungu, na hayo yaliandikwa ili na sisi tujifunze. Neno la Mungu liwe ni namba moja kwako. Ni hatari sana kutegemea vitu vya hapa duniani au kumtegemea mtu.
Sunday, June 16, 2019

UHITAJI WA MACHO YA ROHONI

Mhuburi: Mch. Kiongozi Abdiel Mhini
Maandiko: 2Wafalme 6:8-23

Elisha alikuwa ana macho ya rohoni, alikuwa anajua mipango yote ya Mfalme wa Shamu hata kama akipanga akiwa chumbani kwake, Elisha aliyajua hayo kwasababu alikuwa na macho ya kiroho. 

Elisha alijua mipango ya shamu, ni kwasababu tu alikuwa na Roho Mtakatifu, alikuwa Rohoni. Unahitaji macho ya rohoni kuona vitu vya mbele yako, kuona vitu vya sirini. Kuwa na macho ya Roho kuna faida sana kwasababu utajua hila zote za shetani na mipango yake anayotaka kuitumia kukuangusha.

Tatizo kubwa la wakristo wengi wa sasa ni kutokuwa na muda mzuri wa kukaa na Mungu, kusoma Neno lake na kulitafakari kwa undani, kutumia muda katika kuomba. Ni lazima utengeneze uhusiano wako na Mungu uwe vizuri.

Mathayo 16:23 Yesu hapa aliweza kugundua kama Petro katumiwa na shetani kwasababu alikuwa Rohoni, na akaweza kumkemea kwasababu alikuwa ana nguvu za rohoni. Ili  kuvunja ngome za shetani ni lazima uwe na nguvu za rohoni. Kuna macho ya nyama na macho ya rohoni, jitahidi sana uwe na macho ya rohoni; hila za shetani huwa hazionekani hivi hivi mpaka uwe na macho ya kiroho.

Utapataje Macho ya Rohoni?
  1. Kwa Kusoma Neno la Mungu, bila Neno hutaweza, Ishi katika Roho. Ukiliamini Neno la Mungu linakufungua sana katika ulimwengu wa kiroho na unaanza kuona mambo zaidi.
  2. Kulitii Neno la Mungu, Yohana 9:35-41, unaweza ukalijua Neno lakini usilitii, kutii Neno ndiko kunako badilisha.
  3. Kumwamini Mungu kwa asilimia zote 100% Warumi 4:1-3 Huna macho ya kiroho Kwasababu humwamini Mungu asilimia zote na huamini Neno lake asilimia yote, Abraham alimwamini Mungu kwa asilimia zote, kumwamini Mungu asilimia yote ni kwa muhimu sana, KUNA MAMBO HUTAYAONA MPAKA UTAKAPO AMUA KUMWAMINI MUNGU KABISA KUAMINI ANACHO KWAMBIA, USIWE KIPOFU, JIACHILIE KWA MUNGU, USIWE MKRISTO VUGUVUGU

Sunday, June 9, 2019

KUJAZWA ROHO MTAKATIFU

Mhubiri: Mch. Kiongozi Abdiel M. Mhini
Neno: Matendo 1:1-9

Bwana Yesu aliwaagiza wanafunzi wake kwamba wasitoke mpaka watakapo pokea Nguvu kutoka juu, Yesu anakutaka usitoke mpaka akuvike nguvu kutoka mbinguni, upate nguvu ya Roho Mtakatifu. Wapo watu wamemtafsri Roho Mtakatifu  vibaya wanasema alikuwa kipindi cha huko nyuma tu lakini huo ni uongo, Roho Mtakatifu hata sasa yupo! kipawa hiki kipo kwa ajili yako wewe, pia alikuwepo na yupo hata leo. Ili aingie ndani mwako nil lazima uwe na kiu ya kumpata Roho Mtakatifu.

Sunday, May 26, 2019

WAKATI AMBAPO KULIA HAKUSAIDII

Mhubiri: Mch. Kiongozi Abdiel M. Mhini
Maandiko: 1Samweli 30:1-20

Daudi na watu wake walilia mpaka wakakosa nguvu ya kulia tena, lakini badae akajitia nguvu katika Bwana, akachukua hatua ya kumtafuta Bwana. Katika maisha ya hapa dunia, unaweza kupitia nyakati ngumu, nyakati za majaribu, nyakati za kupungukiwa ukalia sana, lakini je ni unafanya baada ya kulia sana?, hatua gani unachukua baada ya kupata matatizo? Daudu hakuishia tu kulia lakini alichukua hatua ya kumuomba Mungu. Unapopatwa na shida chukua hatua ya kumwambia Mungu, omba kwa Mungu kwa kumaanisha naye atasikia.

Daudi alimuomba Mungu akamuuliza kama akaiwafwatia atawapa? na Mungu akamjibu. Mwambie Mungu shida, Mungu yuko tayari kukusikia naye atajibu atakuonyesha njia ya kupita, atakuelekeza jinsi ya kufanya ili kuondokana na hitaji lako, atakupa majibu ya kweli. Chukua hatua ya kusonga mbele na kuongea na Mungu. 

Acha kulia chukua hatua, Fahamu kuwa hakuna shida yoyote inayomshinda Mungu, Mungu wetu ni Mungu mwenye nguvu sana. Kuwa na muda mzuri wa kuomba, omba kwa bidii, ni lazima utenge muda wako wa kuwasiliana na Mungu wako vizuri na kumueleza, kumuuliza nini ufaye hatua gani uchukue. Mungu akubariki.

Sunday, May 19, 2019

KWANINI YESU ALIKUWA NA BIDII KATIKA KUOMBA

Mhubiri: Mch. Mussa Elias
Maandiko: Marko 1:35-39

Yesu aliamka asubuhi na mapema akaenda sehemu ya faragha KUOMBA. Yesu alikuwa analala sehemu moja na wanafunzi wake kwahiyo wanafunzi walijua alivyoondoka asubuhi na mapema kwenda kuomba. Baadae watu wa pale walikuja kumtafuta ili awahudumie kwahiyo wanafunzi wakamtafuta alipoenda kuomba, wakamwambia watu wanakuhitaji; lakini hapa cha kushangaza, akawaambia twendeni mji mwingine hakutaka tena kuwahudumia watu wa mji ule bali wa mji mwingine, hapa inamaanisha baada ya yale maombi alikuwa ashapata maelekezo ya siku hiyo kutoka kwa Baba yake, hakufanya kama anavyotaka Yeye au mazingira yalivyotaka Bali kama Baba yake anavyotaka. 

Yesu alipenda sana kutenga muda wake mzuri wa kuomba, Yeye alikuwa Mungu asilimia 100% lakini bado aliona kuna umuhimu sana wa kuomba, alipenda kujitenga na kwenda kuomba wakati wa usiku au asubuhi, hapa si maombi ya wote bali maombi binafsi. Je wewe umetenga muda mzuri wa kufanya maombi yako binafsi? Au mpaka maombi ya pamoja kanisani?

Sababu za Yesu kuwa na Bidii katika MAOMBI

1. Yesu alikuwa na mpango maalumu wa kazi ya Mungu (divine plan), alikuwa na 'plan' ndio maana alikuwa anaomba. Ili mipango yako iende vizuri ni lazima uwe na muda wa kuiombea, Yesu alikuwa na kazi mbele yake akaona kuna umuhimu wa kuiombea kwa bidii. Kama mtu una vision/ maono kwa ajili ya kazi ya Mungu ni lazima tu uombe, hapa tunaongolea maombi binafsi. Hapa Yesu alikuwa anafanya maombi binafsi sio ya wote, kama una malengo utakuwa una ratiba yako mwenyew ya kuomba sio mpaka mchungaji atangaze maombi bali lile lengo ndani yako litakuongoza kufanya maombi, Yesu lile lengo ndani yake ndio lilikuwa linamsukuma kuomba akamka asubuhi kuomba mwenyewe. 

- Ukiona huna hamu ya kuomba ujue huna lengo au maono ndani yako.

2. Alikuwa anataka muongozo wa kila siku kutoka kwa Baba yake wa mbinguni. Kutaka muongozo wa kila siku ili ufanye mambo ambayo ni mapenzi ya Mungu uyafanye katika siku hiyo. Ukiongozwa na Mungu kila siku utajua kwa uhakika nini cha kufanya na utafanya vitu sahihi kwa usahihi, sasa unaweza kupata muongozo sahihi katika siku yako kwa kuomba. 

3. Yesu hakutaka kufanya huduma yake kama mambo ya kawaida, bali kwendana na atakavyoongozwa siku hiyo, 'God is not static, God is dynamic, He gives us fresh ideas everyday'. Mungu ana uwezo wa kukupa mawazo mapya kila siku, mawazo mapya ya kufanya kazi zako, ya kufanya biashara zako. Yesu hakutaka kufanya kazi zake kama kawaida, hutakiwi umkariri Mungu bali uwe tayari kufanya anachokuagiza kwa wakati muafaka(flexible).

4. Yesu alitaka kuhudumu kwa usahihi, kwa watu sahihi na sehemu sahihi. Yesu hakuwa anahubiri hubiri tu bali alikuwa ana mpango kamili sasa huwez kufanya hivyo kama huombi. Ili kufanya kitu sahihi na kwa wakati sahihi ni lazima uwe na uongozi wa Mungu atakaye kuelekeza nini cha kufanya na lini.

5. Yesu alikuwa anataka kutekeleza tu atakayoongoza na Baba yake pekee na sio mambo mengine, hata wewe kwenye maisha yako unatakiwa ufanye yale TU unayoongozwa na Roho Mtakatifu na sio vinginevyo. Sasa huwezi kuwa hivyo kama huombi.

6. Kwa Yesu maombi yalikuwa ndio silaha pekee ya kusambaratisha kazi ya shetani, aliweza kufanya kazi kubwa ya kuondoa mapepo na kuponya watu kwasababu alikuwa anaomba vya kutosha, alikuwa anatumia muda mwingi kuomba ndio maana akienda kwenye huduma mapepo na magonjwa yanakimbia. Sasa huwezi kupata upako ule kama huombi, nguvu ile ilikuwa inatengezwa katika maombi.

Kuwa mkristo mwenye nguvu za Mungu hakuji kirahisi tu inakupasa kujitoa mwenyewe kwenye Kusoma Neno na Maombi, kuwa na muda mzuri wa maombi na sio maombi mengi ya juu juu bali maombi ya uhakika.

Sunday, May 12, 2019

RIDHIKA NA ULICHONACHO

Mhubiri: Ndg Leandri Kinabo
Maandiko: Wafilipi 4:10-13

Wafilipi 4:10-13 "kwa maana twajitaabisha na kujitahidi kwa kusudi hili, kwa sababu tunamtumaini Mungu aliye hai, aliye Mwokozi wa watu wote, hasa wa waaminio. 11 Mambo hayo uyaagize na kuyafundisha. 12 Mtu awaye yote asiudharau ujana wako, bali uwe kielelezo kwao waaminio, katika usemi na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi. 13 Hata nitakapokuja, ufanye bidii katika kusoma na kuonya na kufundisha."

Kurithika wakati unapopitia majaribu ni kitendo cha imani, ni kitendo cha kumuamini  kwamba Mungu atakuwezesha. Paulo aliandika sura hiyo alipokuwa gerezani, unaweza kusema alikuwa katika jaribu/ mapito, lakini haikujalisha anapitia hali ngumu kiasi gani, yeye alizidi kumwamini Yesu na kurithika huku akijua kwamba Mungu atamuokoa.

Kutokuridhika huwa kunaanzia ndani ya moyo, unapokosa uhusiano mzuri na Mungu unaanza kuwa na mashaka unaona kama kuna uwezekano Mungu asifanye kitu kuhusu shida yako unayopitia, lakini unapoamua kumwamini Yesu asilimia 100 utakuwa huna hofu  yoyote.

Kuridhika katika Bwana ni tunda la kumwamini Mungu. Ukimwamini Mungu hata kama unapitia katika hali ngumu kiasi gani tambua kuwa Mungu anakupenda na Mungu atafanya kitu kwa ajili yako.