''Badilisha Maisha yako kwa kumpokea Yesu Kristo kuwa Mwokozi wa Maisha Yako.''

Sunday, October 5, 2014

KUISHI MAISHA YA KUMTANGAZA KRISTO

Mhubiri: Christina Daudi
Maandiko: Matendo 23:11, Matendo 4:18-20

Kuishi maisha ya kumtangaza Kristo, Katika maneno hayo tunaona watumishi wa Mungu waliweza kumtanga Kristo katika kipindi chao lakini wakristo wa leo hatuwezi kumtangaza Yesu katika maisha yetu, mienendo yetu, na katika sehemu tunazoishi kwasababu tuna sura za aina mbili. Hizo sura za aina mbili zinatufanya tushindwe kabisa kumuelezea Kristo kwa ujasiri, watakatifu wa siku ya leo wengi wao wamevaa ngozi ya kondoo ndani mmekuwa kama mbwa mwitu, yaani unakuwa huwezi kumtofautisha mtu aliyeokoka na mtu asiyeokoka. Kumbuka umeokolewa ili kutangaza jina la Yesu nyumbani kwako, kazini kwako, shuleni kwako, kila mahali inatakiwa uweze kumtangaza jina la Yesu vizuri ili tuweze kujipatia sifa njema, lakini kama ukaendelea kuishi maisha yenye sura mbili itakupa ugumu wa wewe kulitangaza jina la Yesu. 

Kanuni za kuishi maisha ya kumtangaza Yesu
  1. Ni lazima umjue Yesu unayemtangaza vizuri, inawezekana huwa unaabudu kanisani na watu waliookoka lakini wewe hujawahi kuokoka, usipo okoka hapo utakuwa unajidanganya. Uwe umeliamini Jina la Yesu yaani kuokoka, mtu aliye okoka ana ujasiri na nguvu za kulitangaza Jina la Yesu.
  2. Ni lazima uwe umejaa Neno la Mungu. Huwezi kwenda kuhubiri injili wala huwezi kwenda kumshuhudia mpagani kwa habari ya Yesu kama hutakuwa umejaa Neno la Mungu. Kwahiyo unapaswa kukaa katika Neno la Mungu ulisome ulielewe ili uwe na ujasiri wa kusimama mbele za watu ambao hawajaokoka, ili pale watakapo kubishia wewe useme imeandikwa kama Yesu alivyosema, Yesu alikuwa anasema imeandikwa alivyokuwa akijaribiwa na shetani kwasababu alikuwa amejaa Neno. Ili uweze kumshinda shetani lazima ujae Neno.
  3. Maombi, Inatakiwa umuishie Mungu kwa maombi kwasababu vita vyetu si juu ya damu na nyama bali vita vyetu vipo katika ulimwengu wa roho. Hutaweza kumshinda shetani kama unasubiri mpaka jumapili ndio uje kuomba kwenye ibada. Pata muda wa kuomba binafsi na katika familia yako panga muda maalum wa kuomba, hilo litatusaidia kumshinda shetani na kulitangaza Jina la Yesu kwa ujasiri.
  4. Ni lazima uwe na upendo na huruma, Hayo ndio Yesu aliyoyafanya ndio maana akajitoa uhai wake kwa ajili yetu, alitupenda upeo ili sisi tupate kupona. Ukimpenda mtu ambaye hajaokoka hutaacha kumshuhudia.
  5. Ni lazima uwe umejaa Roho Mtakatifu, hutaweza kuishi maisha matakatifu kama huta kuwa na Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu atakuongoza katika yote.

Miss. Christina Daudi akihubiri kwenye sikukuu ya vijana

No comments:

Post a Comment