''People are being transformed into Jesus Christ through faith and the word of God''

Sunday, August 16, 2015

UHURU WA KIROHO

Mhubiri: Mch. Elias Mussa
Maandiko: Yohana 8:30-32

Kila kitabu kwenye biblia kiliandikwa kwa kusudi fulani na kusudi la injili ya Yohana inapatikana katika Yohana 20:31, kimeandikwa ili upate kuamini ya kwamba Yesu ndiye Kristo Mwana wa Mungu; na kuamini mwe na uzima kwa jina lake. Kwahiyo ukikisoma kitabu cha Yohana kumbuka kwamba kazi yake ni kukufanya uamini kuwa Yesu ni Kristo ili uwe na uzima wa milele.

Lakini leo tumesoma Yoh 8:30-32 ambayo sura hii yote inaongelea Yesu kuwa ni Nuru ya ulimwengu na pia kwasababu kusudi la kitabu cha Yohana ni kukufanya wewe uamini, inawasema wale waliomwamini Yesu, Yesu alikuwa anawaambia wayahudi ndio mmeniamini lakini hiyo haitoshi kuamini hivyo tu bali kuna vitu vingine unatakiwa kuvifanya. Ndio umeshamwamini Yesu na ukaokoka lakini haitoshi kuishia hapo bali kuna mambo mengine ya kufanya ili uwe na uhuru kweli kweli wa kiroho. Na uhuru wa kiroho ni wa muhimu sana na ni mzuri hakuna mtu ambaye hapendi kuwa huru.

Sasa uhuru huwa hauji hivi hivi, Tanganyika tulitawaliwa lakini baada ya kufanya mambo fulani tukapata uhuru wetu, hivyo hivyo katika mambo ya kiroho ili uwe huru kabisa kiroho lazima ufanye mambo yafuatayo:
  1. KUAMINI, ili uwe huru kiroho lazima uamini kwamba Yesu Kristo ni mwana wa Mungu. Kuna wale wanaoamini kwamba Yesu alikuwa ni mtu tu kama sisi, watu kama hao wanaoamini hivyo hawawezi kuwa huru kiroho. Kuamini ni kukubaliana na Mungu kwamba anachosema kuhusu yeye mwenyewe ni kweli, lakini nini anachosema kuhusu Yeye mwenyewe ni kwamba Yeye ni nuru ya ulimwengu. Pia kukubali kuwa anachokisema kuhusu wewe ni kweli, akisema wewe ni mwenye dhambi na ukakubali kuwa wewe ni mwenye dhambi hapo ndipo kutakuwa mwanzo wa uhuru wako. Kwahiyo ukiamini anachosema kuhusu yeye mwenyewe ni kweli na anachosema kuhusu wewe ni kweli hapo ndipo kutakuwa mwanzo wa uhuru wako kiroho. Yawezekana kuwa huwa hukubali kuwa wewe ni mwenye dhambi, na unapokataa tu kuwa wewe sio mwenye dhambi hutapata kamwe uhuru wa kiroho. Unapokubali na kuamini kuwa Yesu ni mwokozi utawekwa huru lakini ukiamini kuwa Yesu alikuwa kama mtu wa kawaida tu hutawekwa huru.
  2. KUKAA KATIKA NENO LA MUNGU, lazima usome Neno lakini sio hivyo tu bali unatakiwa kuendelea kukaa katika Neno. Sasa hivi kuna wakristo wanaokuja kanisani lakini wamejazwa mapepo ndani ni kwasababu hawasomi Neno la Mungu. Ukiacha tu kusoma Neno la Mungu hata kama umeokoka utakuwa mtumwa tu, yawezekana unazunguka makanisa mbali mbali kutafuta uponyaji au Baraka lakini hutapata wala pia hutakuwa huru kiroho mpaka utakapoamua kuanza kusoma Neno la Mungu kwa uaminifu na kukaa na Neno la Mungu. Kusoma Neno la Mungu iwe ndio maisha yako na hapo ndipo utakuwa mwanafunzi wa Yesu, huwi mwanafunzi wa Yesu kwa kuombewa lazima Neno lake likae ndani yako na wewe uwe ndani yake ili uwew mwanafunzi wa Kristo, na ukiwa sasa mwanafunzi wa Kristo ndipo utakuwa huru. Huwezi kuwa huru kiroho bila kuwa mwanafunzi wa Kristo.
  3. LAZIMA UJUE KWELI, Unapoendelea kukaa katika Neno la Mungu utaanza kujua kweli na hiyo kweli sasa ndiyo utakuweka huru kweli kweli. Na utakapojua kweli fahamu zako zitakuwa hai. Na hiyo kweli itakubadilisha utaanza kuelewa vitu vizuri kama Mungu anavyotaka uelewe na hapo hakuna mtu atakayeweza kukubabaisha tena au kukuchanganya kwa lolote. Kweli itakuwa sehemu ya maisha yako wala hutaweza kudanganya. 

No comments:

Post a Comment