''Badilisha Maisha yako kwa kumpokea Yesu Kristo kuwa Mwokozi wa Maisha Yako.''

Wednesday, July 6, 2016

USIWE NA MIUNGU MINGINE ILA MIMI

Mhubiri: Frank Mwalongo
Maandiko: Kutoka 20:1-7
 
 "1 Mungu akanena maneno haya yote akasema,2 Mimi ni Bwana, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa. 3 Usiwe na miungu mingine ila mimi. 4 Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. 5 Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, Bwana, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao, 6 nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri zangu. 7 Usilitaje bure jina la Bwana, Mungu wako, maana Bwana hatamhesabia kuwa hana hatia mtu alitajaye jina lake bure."
 
UTANGULIZI
Maandiko kutoka katika kitabu hiki yanaelezea jinsi wana wa Israeli walivyosafiri kutoka Misri kwenda Kaanani. Kama tunavyofahamu Mungu alitenda makubwa kuwatoa kutoka Misri hata kufika katika mji wa ahadi. Katika sura hii ya ishirini Mungu alimwita Musa na kuzungumza naye kwa habari ya watu hawa  walio safarini kwenda mji wa ahadi.
 
Katika safari ya wana wa Israeli kuelekea katika mji wa ahadi njiani Mungu aliangalia mioyo yao na kuona kwamba bado mioyo yao haijamgeukia Yeye na badala yake bado wamebeba miungu ya Misri. Akamuita Musa juu mlimani na kuzungumza naye kwa habari ya wana hawa wa Israeli. Akamwambia akawaambie wana wa Israeli maneno haya kutoka katika kitabu cha kutoka sura ya 20 mstari wa 1 hadi wa 7.
 
Lakini wana wa Israeli baada ya kumsubri Musa kwa muda bila mafanikio ya kumuona waliamua kujenga sanamu na kuiabudu kama mungu wao, (KUTOKA 32:1-8). Baada ya Musa kufika chini ya mlima alipowakuta wakiabudu sanamu hasira yake iliwaka hata akavivunja vibao alivyopewa na Mungu mikononi mwake,(KUTOKA 32:15-24).
 
Chochote ulichoshikilia na kukitumikia hiko ni kinyago(sanamu) na Mungu anasema kuwa usiwe na miungu mingine ila Mimi. Hata jumapili sasa imekuwa na muda kidogo sana kwa ajili ya Bwana na muda uliobaki unatumika kufanya mambo mengine, hayo mambo mengine ni vinyago(sanamu) ambavyo vinakuzuia kukutana na Mungu.

Musa alifanikiwa kurudi na kuongea tena na Mungu kwa habari ya wana wa Israeli, na hatimae safari iliendelea, (KUMBUKUMBU LA TORATI 4:22-24). Lakini walipofika Kaanani bado waliendelea kukumbatia vinyago vyao (sanamu). Yoshua nao aliagizwa na Bwana kuongea na wana wa Israeli kwa habari ya kuchagua ni nani watakae mtumikia, (YOSHUA 24:14-15,YOSHUA 23:12-14).
 
Chochote kisichokuwa cha Roho Mtakatifu ni kinyago mbele za Mungu. Chochote kinachochukua nafasi ya Mungu katika maisha yako ni kinyago mbele za Mungu. Katika siku za leo kuna muingiliano mkubwa sana kati ya watu wa mataifa na watumishi wa Mungu, nyuma ya muingiliano huu kuna dhambi. Ndio maana siku za leo makanisani nyimbo zinazoimbwa zinakuwa za muingiliano kati ya madhabahu ya  shetani na ya Mungu kwa kuwa nyimbo hizi zinakuwa na ala ya shetani. Kuchukua nyimbo zilizo katika madhabahu ya shetani ni kukaribisha mapepo ya dhambi kutoka katika madhabahu ya shetani ndani ya nyumba ya Mungu.
 
JIKAGUE SIKU YA LEO NA UANGALIE, "NI KITU GANI KIMECHUKUA NAFASI KULIKO MUNGU AMBACHO UKIKISIKIA KINAKUFANYA UACHE MAMBO YA MUNGU NA KUKIKIMBILIA?"
Baada ya kujua na kutambua kitu hicho, Jua sasa kuwa ni kinyago mbele za Mungu ambacho Mungu anasema kuwa usiabudu Mungu mwingine ila yeye tu.
 
 
 

No comments:

Post a Comment