''People are being transformed into Jesus Christ through faith and the word of God''

Sunday, January 22, 2017

KAA MIGUUNI PA YESU

Mhubiri: Mch. Kiongozi Abdiel M. Meshark
Maandiko: Luka 10:38-42

Ili wewe uendelee kiroho lazima ukae na kumsikiliza Yesu na hili ndilo Maria alilofanya. Ndio kumuandalia mgeni kitu akija kwako sio kitu kibaya wala hatusemi uache kufanya hivyo, lakini hapa somo lilikuwa ni kwanini ratiba yako imejaa sana mpaka huna muda wa kukaa na Yesu?. Je ni kwa kiasi gani umeamua kukaa karibu na Mungu?, Maria alichagua kilicho bora je wewe kipi bora kwako?.

Hapa tunajifunza kwamba tunaye Yesu Kristo, kiongozi wetu, lakini ni kiasi gani tunakaa nae karibu, ni kwa kiasi gani una ushirika naye?.
 
Mojawapo ya njia za kukaa karibu na Mungu ni kusoma Biblia, sasa je una mpango maalum wa kusoma Biblia katika mwaka mzima au ratiba yako imejaa tu vitu visivyo vya Mungu?. Siku hizi kuna mafundisho mazuri sana yanayopatikana kwa walimu wazuri kupitia vitabu na mtandao, sasa je ni kwa kiasi gani unayafwatilia au huwa unatumia mtandao kuchati tu.
 
Kushikamana na Mungu yaani kukaa miguu pa Yesu ni kitu cha muhimu sana katika maisha yako. Kutoka 33:13 "Basi, sasa nakuomba, ikiwa nimepata neema mbele zako, unionyeshe njia zako, nipate kukujua, ili nipate neema mbele zako; ukakumbuke ya kuwa taifa hilo ndilo watu wako". Mussa alivyopewa kazi ya kuwapeleka wana wa Israel, akamuomba Mungu kama kapata kibali amfundishe ili amjue Mungu zaidi na Mungu akamwambia uwepo wake utakuwa nae, sasa Je wewe unatamani nini? Je unatamani Mungu akufundishe zaidi na zaidi?

 
Isaya 42:9 "Tazama, mambo ya kwanza yamekuwa, nami nayahubiri mambo mapya; kabla hayajatokea nawapasheni habari zake." Faida mojawapo ya kukaa na Yesu, atakuambia na kukuonyesha vitu vya kufanya kama utakuwa na muda nae mzuri.
 
Yohana 15:4 "Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu." Kama Utaishi bila uwepo wa Mungu vitu vyote utakavyofanya vitakuwa hasara. Hatuwezi kufanya kitu bila kukaa ndani ya Yesu, bila uongozi wa Roho Mtakatifu hutaweza kufanya kitu utakuwa kama mti usio zaa. Pia pale utakapoamua kwa kumaanisha kukaa miguuni pa Yesu, Yesu atajionyesha kwako, unapoamua kulitangaza jina la Yesu kwa watu Mungu hatakuacha kwasababu umeamua kufanya kazi yake.
 
Ibada binafsi ya kutaka kumuona au kuona uwepo wa Mungu ni ya muhimu sana, zaburi 27:4 "Neno Moja nimelitaka kwa Bwana, Nalo ndilo nitakalolitafuta, Nikae nyumbani mwa Bwana Siku zote za maisha yangu, Niutazame uzuri wa Bwana, Na kutafakari hekaluni mwake." Mfalme Daudi alitamani kuendelea kumtafuta Mungu na kukaa katika nyumba ya Mungu, Je wewe unatamani hilo, na kwa kiasi gani unatamani hilo?. Ibada inaanzia kwako binafsi.
 
Upendo na uzuri wa Mungu utauona tu kama ukiamua kukaa na Yesu, amua leo kwa kumaanisha kutoka moyoni kukaa karibu na Mungu.

No comments:

Post a Comment