''Badilisha Maisha yako kwa kumpokea Yesu Kristo kuwa Mwokozi wa Maisha Yako.''

Monday, May 14, 2018

MPENDE JIRANI YAKO KAMA NAFSI YAKO

Mhubiri: Mr. Frank Mwalongo
Neno: Walawi 19:1-2,18, Kutoka 20:17

Hili agizo/amri ya kumpenda jirani yako kama nafsi yako limeanzia tangu agano lake, na hii ndio amri kuu ya pili katika zile alizozisema Yesu katika Mathayo 22:36-39 "Mwalimu, katika torati ni amri ipi iliyo kuu? 37 Akamwambia, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. 38 Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. 39 Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako."

Hizi amri mbili kuu zinatoa muhtasari wa mafundisho yote ya Yesu, Mafundisho yote ya Yesu yalifundisha pande kuu mbili ambazo ni kumpenda Mungu na kumpenda jirani yako kama nafsi yako. Hapa tutaangalia zaidi amri ya pili; kumpenda jirani yako kama nafsi yako.

Ili uweze kumpenda jirani yako kama wewe mwenyewe unavyojipenda ni lazima uwe na unyenyekevu , hali ya kujishusha, uwe mtu wa kusamehe wengine, mtu mwenye kuwahurumia wengine. Ili uweze kumpenda jirani yako kama unavyojipenda wewe ni lazima uamue kufanya hivyo maana mara nyingi nafsi yako itakufanya kujiangalia wewe mwenyewe zaidi ya mwenzako.

Ni muhimu sana kumpenda jirani yako kama nafsi yako na Neno la Mungu limeweka wazi kabisa jambo hilo katika Marko 12:33 "na kumpenda yeye kwa moyo wote, na kwa ufahamu wote, na kwa nguvu zote, na kumpenda jirani kama nafsi yako, kwafaa kuliko sadaka nzima za kuteketezwa na dhahibu zote pia." Kwahiyo ni muhimu sana kumpenda mwenzako kuliko kutoa sadaka kanisani, kwa maana nyingine ukiwa unamchukia mwenzako una kinyongo na mwenzako, sadaka yako ni bure Mungu hataipokea. Hata kama mtu anakuudhi mpende jinsi alivyo na msamehe usimuweke moyoni.

Pia, Biblia inazidi kuelezea umuhimu wa hii amri ya kumpenda jirani yako, na ya kwamba sheria yote imeshikiliwa hapo, Galatia 5:14 "Maana torati yote imetimilika katika neno moja, nalo ni hili, Umpende jirani yako kama nafsi yako." Kwahiyo kama hutampenda mwenzako utakuwa unatoka nje ya maagizo ya Mungu.

Unaweza ukawa unajiuliza, Jirani ni nani?, hili swali wanafunzi walishawahi kumuuliza Yesu na akawajibu vizuri katika Luka 10:29-37 kuhusu yule msamaria aliyemsaidia mtu aliyeumizwa na wezi njiani. Kwahiyo, Jirani ni mtu yeyote yule utakaye kutana nae katika mazingira yako, sio lazima uwe unamfahamu. Yule msamaria hakumfahamu yule mtu alimkuta tu njiani lakini alimuonea huruma, akamsaidia.

Na kiwango cha kumpenda jirani yako kimewekwa wazi kabisa, ya kwamba; umpende jirani yako Kama Nafsi Yako. Kama unavyojipenda wewe mwenyewe ndivyo umpende mwenzako. Kwahiyo anza leo kuwapenda wenzako kama unavyojipenda wewe.

1 comment:

  1. Nashukuru sana baba kwa mafundisho mazuri. Nimepata kitu maishani meangu

    ReplyDelete