''Badilisha Maisha yako kwa kumpokea Yesu Kristo kuwa Mwokozi wa Maisha Yako.''

Sunday, August 19, 2018

SISI NI NURU YA ULIMWENGU

Mhubiri: Ndg. Frank Mwalongo
Maandiko: Yohana 1:6-9, 8:12, Mathayo 5:14-16 

Kazi ya kuu ya Yohana mbatizaji ilikuwa ni kuiandaa dunia kupokea Nuru, ambayo Nuru yenyewe ni Yesu Kristo. Yesu Kristo ni nuru ya ulimwengu. Ilibidi Nuru ije kwasababu ulimwenguni kulikuwa na giza, kila mtu ndani yake alikuwa amejaa giza.

Katika Yoh 8:12, "Basi Yesu akawaambia tena akasema, Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima." Hii ilikuwa ni hotuba ya kwanza ya Yesu, anajitambulisha kuwa Yeye ni nani. Anauambia ulimwengu ulio na shida kwamba yeyote atakayemfuata hatakuwa gizani kamwe bali nuruni. Kwa maana nyingine baada ya kuja Yesu wokovu ukaja. Habari kuu ya Yesu ni kutoka kwenye giza kwenda kwenye nuru.

Unapookoka, Unapompokea Yesu, unapokea nuru ndani yako, unaanza kuwa na nuru maishani mwako, unakuwa huru kweli kweli, unaanza kuishi maisha matakatifu ya kuishinda dhambi kwasababu dhambi inakuwa haikutawali tena giza limeondoka ndani mwako.

Sasa basi, wewe kama mtu uliyeokoka/ uliyepokea Nuru na ukawa nuru, nuru hiyo unapaswa uiangaze kwa watu. Mathayo 5:14-16, taa ikiwashwa inawekwa juu ili iangaze sehemu yote, vivyo hivyo na wewe nuru uliyonayo iangaze mbele za watu, ili kupitia wewe, kupitia maisha yako watu wakamjue Yesu, wamtukuze Baba yako aliye mbinguni. Jinsi tu unavyoishi na watu, jinsi maisha yako yalivyo ni ushuhuda tosha wa kumtangaza Yesu, kwasababu watu wataona tu matendo yako ni ya tofauti, kwamba huna tena matendo ya giza bali ya nuru. Wewe ni mtu wa kuigwa, watu ambao bado wako kwenye giza wajifunze kutokana na matendo yako ya nuru, wavutiwe na ile nuru. Sasa swali kubwa la kujiuliza, Je, ni kweli matendo yako yanamuwakilisha Yesu ambaye ni Nuru? Je, matendo yako yanamtukuza Mungu?

No comments:

Post a Comment