''Badilisha Maisha yako kwa kumpokea Yesu Kristo kuwa Mwokozi wa Maisha Yako.''

Sunday, May 18, 2014

IMANI IAMBATANAYO NA MATENDO

Mhubiri: Mchungaji Kiongozi Mhini

Baada ya Bwana Yesu kufufuka katika wafu, aliwatokea wanafunzi na watu wengine maeneo mbalimbali. Aliwatokea kwa muda wa siku arobaini na kuyanena mambo yaliyouhusu Ufalme wa Mungu. Lakini agizo alilowaagiza wanafunzi ni kwamba wasitoke Yerusalemu bali waingoje ahadi ya Baba ambayo walisikia habari zake kwake; ya kwamba watabatizwa kwa Roho Mtakatifu siku chache baadaye (Mdo 1: 2-5).

Bwana Yesu alilitimiza agizo lake ilipotimia siku ya Pentekoste, yaani siku ya hamsini tangu amefufuka katika wafu (Mdo 2: 1-13). Pale ambapo wote waliokusanyika walijazwa Roho Mtakatifu, na kuanza kusema kwa lugha nyingine kama Roho alivyowajaalia kutamka.
Tendo kubwa la muujiza na ajabu la kwanza kwa wale waliojazwa Roho Mtakatifu siku ile, ni ile hotuba ya Petro aliyoitoa kwa watu wa Uyahudi na wakaazi wa Yerusalemu waliolipokea Neno lake wakapata kubatizwa watu elfu tatu. Nao wakawa wakidumu katika fundisho la Mitume na katika ushirika, na katika kumega mkate, na katika kusali (Mdo 2: 14 - 42).

Katika safari za Paulo za Umisheni, alifika Efeso na kuwakuta wanafunzi kadha wa kadha, ambao walikuwa bado hawajajazwa Roho Mtakatifu tangu walipoamini na wala kusikia habari zake. Paulo alichukua hatua ya kuwawekea mikono na Roho Mtakatifu alikuja juu yao; nao wakaanza kunena kwa lugha na kutabiri, idadi yao walikuwa kumi na wawili (Mdo 19: 1-7). Hili tukio lilitokea miaka 25 baada ya Pentekoste. 

Mungu kwa mikono ya Paulo alifanya miujiza mingi ili litimie lile Neno alilolinena Bwana Yesu katika kitabu cha Marko kwamba “Enendeni ulimwenguni mwote mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe, aaminiye na kubatizwa ataokoka, asiyeamini atahukumiwa. Bwana Yesu aliahidi ishara zitafuatana na hao waaminio. Kwamba kwa jina la Yesu, watyatoa pepo, watasema kwa lugha mpya, wataweka mikono yao juu ya wagonjwa nao watapata afya (Mark 16:15-18).

Huduma ya Paulo katika Efeso, ilithibitishwa na miujiza ya uponyaji, kutoa pepo kwa leso toka mwilini mwake (Mdo 19: 11-12). Mhubiri yeyote anayetumia leso kupata faida ya fedha na mali ili afaidike, anakosea, haendi na nia ya leso ya Paulo. Paulo aliyatenda hayo ili Bwana Yesu azidi kutukuzwa.

No comments:

Post a Comment