''People are being transformed into Jesus Christ through faith and the word of God''

Sunday, July 1, 2018

CHOCHOTE KINACHOTOKEA, NI KWA UTUKUFU WA MUNGU

Mhubiri: Ndg. Frank Mwalongo
Maandiko: Kutoka 14:5-29, 1Petro 5:10-11

Mungu alimfanya Farao ajilaumu kwanini amewaruhusu Waisraeli waende, akaamua kuwafuata. Farao akaamua kujiandaa kweli kweli akapanga kikosi cha farasi 600 wa vita na askari wake wengine wote wakafuata, lakini huko mbeleni utaona kilichomkuta. 

Sasa wakati huo Waisrael walikuwa wakitembea wakijiamini tu lakini walipogeuka nyuma na kuona lile jeshi la Farao linawafuata na mbele kuna bahari kujiamini kwao kukaisha, wakaogopa sana, wakaanza kulalamika kwa Musa, angalia maswali waliyoanza kumuuliza Musa; Kutoka 14:11-12 "Wakamwambia Musa, Je! Kwa sababu hapakuwa na makaburi katika Misri umetutoa huko ili tufe jangwani? Mbona umetutendea haya, kututoa katika nchi ya Misri? Neno hili silo tulilokuambia huko Misri, tukisema, Tuache tuwatumikie Wamisri? Maana ni afadhali kuwatumikia Wamisri kuliko kufa jangwani."  Yawezekana na wewe unaangalia hali ngumu unayopitia, huoni njia unaanza kupata woga kwamba itakuwaje unaanza kujiuliza maswali mengi, huo ni woga.

Kitu chochote kinachotokea kwenye maisha yako kama mtu wa Mungu usiogope wala huna haja ya kuogopa kwasababu, vyote vinavyotokea vinatokea kwasababu ya utukufu wake Mungu, wewe endelea mbele!. 

Kwenye mstari wa 17-18, Mungu anasema wazi kabisa lengo la hilo; Kut 14: "17 Nami, tazama, nitaifanya mioyo ya Wamisri kuwa migumu, nao wataingia na kuwafuatia, nami nitajipatia utukufu kwa Farao, na kwa jeshi lake lote, kwa magari yake na kwa wapanda farasi wake. 18 Na Wamisri watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, nitakapokwisha kujipatia utukufu kwa Farao, na magari yake, na farasi zake." Kwahiyo usilalamike na kujuta, kupitia hiyo hali uliyopo Mungu atajipatia utukufu.

Neno la Mungu linasema endelea mbele utukufu wa Mungu upo pamoja nawe utaonekana tu, utukufu wa Mungu huwa upo tayari kwa ajili yako unachosubiri ni ule udhihirisho wake tu. Hebu tutembee kwa kujiamini Mungu wetu ni Mkuu, mara nyingi tunakosea kwababu ya mtazamo mbaya unasizani kama Mungu ni mdogo au ni wa kawaida, Mungu ni mkuu sana, utukufu wa Mungu ni mkuu sana (Wagalatia 1:5), hebu acha kuwa na woga endelea mbele hata kama bado hujaona muujiza wako kwa macho wewe endelea mbele Kutok 14:18. Ubarikiwe.

No comments:

Post a Comment