Mhubiri: Mchungaji Kiongozi Mhini
Baada ya Bwana Yesu
kufufuka katika wafu, aliwatokea wanafunzi na watu wengine maeneo mbalimbali.
Aliwatokea kwa muda wa siku arobaini na kuyanena mambo yaliyouhusu Ufalme wa
Mungu. Lakini agizo alilowaagiza wanafunzi ni kwamba wasitoke Yerusalemu bali
waingoje ahadi ya Baba ambayo walisikia habari zake kwake; ya kwamba
watabatizwa kwa Roho Mtakatifu siku chache baadaye (Mdo
1: 2-5).
Bwana Yesu
alilitimiza agizo lake ilipotimia siku ya Pentekoste, yaani siku ya hamsini
tangu amefufuka katika wafu (Mdo 2: 1-13).
Pale ambapo wote waliokusanyika walijazwa Roho Mtakatifu, na kuanza kusema kwa
lugha nyingine kama Roho alivyowajaalia kutamka.
Tendo kubwa la
muujiza na ajabu la kwanza kwa wale waliojazwa Roho Mtakatifu siku ile, ni ile
hotuba ya Petro aliyoitoa kwa watu wa Uyahudi na wakaazi wa Yerusalemu
waliolipokea Neno lake wakapata kubatizwa watu elfu tatu. Nao wakawa wakidumu
katika fundisho la Mitume na katika ushirika, na katika kumega mkate, na katika
kusali (Mdo 2: 14 - 42).
Katika safari za
Paulo za Umisheni, alifika Efeso na kuwakuta wanafunzi kadha wa kadha, ambao
walikuwa bado hawajajazwa Roho Mtakatifu tangu walipoamini na wala kusikia
habari zake. Paulo alichukua hatua ya kuwawekea mikono na Roho Mtakatifu
alikuja juu yao; nao wakaanza kunena kwa lugha na kutabiri, idadi yao walikuwa
kumi na wawili (Mdo 19: 1-7). Hili tukio
lilitokea miaka 25 baada ya Pentekoste.
Mungu kwa mikono ya
Paulo alifanya miujiza mingi ili litimie lile Neno alilolinena Bwana Yesu
katika kitabu cha Marko kwamba “Enendeni ulimwenguni mwote mkaihubiri Injili kwa
kila kiumbe, aaminiye na kubatizwa ataokoka, asiyeamini atahukumiwa. Bwana Yesu
aliahidi ishara zitafuatana na hao waaminio. Kwamba kwa jina la Yesu, watyatoa
pepo, watasema kwa lugha mpya, wataweka mikono yao juu ya wagonjwa nao watapata
afya (Mark 16:15-18).
Huduma ya Paulo
katika Efeso, ilithibitishwa na miujiza ya uponyaji, kutoa pepo kwa leso toka
mwilini mwake (Mdo 19: 11-12). Mhubiri
yeyote anayetumia leso kupata faida ya fedha na mali ili afaidike, anakosea,
haendi na nia ya leso ya Paulo. Paulo aliyatenda hayo ili Bwana Yesu azidi
kutukuzwa.
No comments:
Post a Comment