''Badilisha Maisha yako kwa kumpokea Yesu Kristo kuwa Mwokozi wa Maisha Yako.''

Sunday, November 6, 2016

JE, MOYO WAKO UMEUELEKEZA WAPI?

Mhubiri: Mch. Kiongozi Abdiel Meshark Mhini
Maandiko: Ezra 7:1-10, Ezra 8:15-21


Uhusiano wako na Mungu unategemea sana na mahali ulipouelekeza moyo wako, hii ikimaanisha kwamba kwa njia ya maombi na kusoma Neno la Mungu, kwa kuyafanya haya mawili ndivyo utakavyokuwa unampa nafasi Roho Mtakatifu ya kubadilisha maisha yako kuwa ya kiroho zaidi.
 
Tunamuona Ezra, kuhani Mungu alimtumia zaidi kwasababu moyo wake aliuelekeza kwa Mungu. Ezra alikuwa kati ya wana wa Yuda waliopelekwa uhamishoni Babeli. Hapa tuliposoma ni wakati Ezra ameshekuwa kuhani na kiongozi wa kundi la pili la wana wa Israel, akiwaongoza wana wa Israel kutoka utumwani Babeli kurudi nchi yao ya Yuda.
 
Sasa Ezra huyu kuhani na mwandishi alifanikiwa sana katika kuliongoza kundi lile la pili alilokuwa nalo, na kati ya kitu kimoja alichosimama nacho sana Ezra ni kuhakikisha kundi lile liko takatifu muda wote lisilo na mawaa, kusanyiko linalompendeza Mungu. Lakini kukawa na kosa kubwa sana limefanyika, lile kundi likaingia uasi kwasababu lilioa wanawake wa kigeni kama wagiligali, waperizi, wahiti na wakanani; walichangamana nao na kuzaa nao watoto, hilo lilimuhuzunisha sana Ezra.
 
Ezra akakasirika sana akakusanya lile kundi  akiwauliza kwanini wamechangamana na wanawake waabudu sanamu?, na ndivyo ilivyo sasa watu waliookoka wanaotaka kwenda mbinguni lakini mguu mmoja bado uko duniani, hamwangalii tena Mungu aliye waokoa, mguu mmoja duniani mguu mwingine wanasema mimi nimeokoka lakini matendo yao hayaambatani na wokovu wanaousema maishani mwao, wanakwenda katika njia za dunia wanajichanganya na dunia, wanakwenda katika misingi Mungu aliyoikataa.
 
Ndugu yangu kujichanganya ni kubaya, ukishaambiwa wewe ni mwana wa Mungu, umeokolewa kwa damu ya Bwana Yesu, haikupasi tena kujichanganya na dunia, jitambue wewe ni mtu uliyetengwa kwa kazi maalum kwamba umewekwa wakfu na Bwana, kwanini kuikumbuka tena dunia?, kwanini kuyakumbuka maasi ya dunia hii? ulishakwisha kuoshwa kwa damu ya thamani ya mwana kondoo Yesu Kristo.
 
Je uko wapi leo, unaposoma ujumbe huu moyo wako umemuelekuzea nani leo?, je umemuelekezea Mungu au dunia?, je una utetea vipi wokovu wako?, mbona unafanya mambo ya kumuhudhunisha Mungu, mwingine anakosa ibada kwasababu ya kwenda kuangalia mechi ya mpira tu! hata wanaocheza hawamjui lakini amekosa ibada kisa mpira, ukimuuliza anasema leo kuna mechi bhana, anaona ni afadhali akaangalie mechi kuliko Mungu aliyenae, na kuna mifano mingine mingi inayofanana na huo wa kukipa kitu flani kipao mbele zaidi ya Mungu aliyekuokoa, huu ni uasi mkubwa mbele za Mungu sio jambo zuri hata kidogo.
 
Ezra alielekeza moyo wake katika kutafuta sheria za Bwana, siku ya leo je, ni kwa kiasi gani mpendwa unayatafuta mapenzi ya Mungu na kuyaenenda? na kupenda maagizo ya Mungu? Wokovu sio jambo la mchezo, kwanini unauchezea wokovu wako? wakati umeshatengwa na dunia, yanini kuyafuata tena mambo ya dunia? Kwanini umepunguza thamani ya Yesu Kristo ndani yako?. Ndugu yangu amua leo kugeuka na kumrudia Mungu na uanze kuishi nae kwa uaminifu.

No comments:

Post a Comment