Maandiko: Hesabu 13:1-33
Wana wa Israel wakiwa kwenye nyika ya Parani karibu kabisa na nchi walio ahidiwa Kanaani, Bwana akamwambia Mussa atume watu kutoka kwenye kila kabila wakaipeleleze nchi ya kanani, na Mussa akafanya hivyo.
Wapelelezi wale waliambiwa wakaichunguze Kanaani vitu vifwatavyo
1. Kwamba watu wanaokaa huko ni hodari au dhaifu
2. Kwamba ni wachache au wengi
3. Kwamba nchi hiyo ni njema au mbaya
4. Kwamba watu wa huko wanakaa katika matuo au ngome
5. Kwamba ni nchi ya unono au njaa
Lakini pia wakalete matunda ya nchi hiyo. Wakatumia siku 40 kuichunguza.
Waliporudi, walitoa ripoti na sio mbele ya Mussa peke yake bali mbele za watu wote. Hebu tuangalie ripoti ile hatua kwa hatua,
Tunaona mwanzo wa ripoti wana wa Israel walifurahi; mstari wa 27
"27.Wakamwambia wakasema, Tulifika nchi ile uliyotutuma, na hakika yake, ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali, na haya ndiyo matunda yake."
Lakini mstari wa 28-29
"28 Lakini watu wanaokaa katika nchi ile ni hodari, na miji yao ina maboma, nayo ni makubwa sana; na pamoja na hayo tuliwaona wana wa Anaki huko. 29 Amaleki anakaa katika nchi ya Negebu; na Mhiti, na Myebusi, na Mwamori wanakaa katika milima, na Mkanaani anakaa karibu na bahari; na kando ya ukingo wa Yordani."
Watu wakaanza kuogopa na kupata hofu lakini mstari wa 30 Kalebu mtumishi wa Mungu akatoa neno la imani ili liwatoe watu hofu
"30 Kalebu akawatuliza watu mbele ya Musa, akasema, Na tupande mara, tukaitamalaki; maana twaweza kushinda bila shaka."
Kalebu alimwamini Mungu kwamba wataweza kushinda bila shaka, lakini kwenye mstari wa "31 Bali wale watu waliopanda pamoja naye wakasema, Hatuwezi kupanda tupigane na watu hawa; kwa maana wana nguvu kuliko sisi." wapelelezi wenzake wanampinga kwamba haiwezekani.
Kanaani siku ya leo ni kwenda katika ukamilifu wa ahadi za Mungu, tunatakiwa tupige hatua za imani, wana wa Israel walitakiwa wamfuate au wawaze kama Kalebu. Baada ya kuokolewa kuna mambo yanayokuja mbele yako ambayo yanaonekana kama ni magumu lakini hapo ndipo sehemu ya kupiga hatua ya ki-imani, unapopita katika majaribu ni mahali sahihi ya kukuza imani yako. Unapoona kuna jambo gumu mbele yako ni muda sahihi wa kumwamini Mungu zaidi, usimlinganishe Mungu na kitu chochote.
Maana ya ripoti ya wale wapelelezi 11 ni kwamba waliona kwamba yale majitu ya Kanaani wana nguvu kuliko Mungu wao badala ya kukumbuka jinsi Mungu wao alivyowapigania na kuwatetea na kwamba ataweza kuwatetea na kuwashinda watu wa Kanaani.
Tusimame kwenye ripoti ya Kalebu, Mungu anaweza kufanya kila kitu ana uwezo wa kukupa kila hitaji lako, lakini je unamwamini kwamba anaweza?, usitishwe na mambo anayokuletea shetani mbele yako au watu wanavyosema juu yako wewe mwamini Mungu tu. Mungu ndio jibu la kila kitu katika maisha yako. Usitegemee akili zako mwenyewe, muda mwingine unaweza kupita katika jaribu ambalo kwa akili za kibinadamu haliwezekani lakini tambua kwamba Mungu analiweza, hebu amua leo kumwamini Mungu kwa asilimia zote kwamba anaweza kukutoa katika hali hiyo.
No comments:
Post a Comment