''Badilisha Maisha yako kwa kumpokea Yesu Kristo kuwa Mwokozi wa Maisha Yako.''

Sunday, April 7, 2019

UNAPO BARIKIWA NA BWANA, USIMSAHAU MUNGU WAKO

Mhubiri: Mch. Kiongozi Abdiel M. Mhini
Maandiko: Kumb la torati 8:6-20, Mithali 30:7-9 

Mungu alikuwa anawaandaa wana wa Israel kuingia katika nchi aliyo waahidi, nchi ya ahadi yenye maziwa na asali. Kwasababu ya uzuri wa nchi ile, watakapo ingia watafanikiwa sana, sasa hapo watakapo fanikiwa sana wasimuache Mungu na kusahau Mungu alipowatoa, wasiabudu miungu mingine bali wamwabudu Mungu wa kweli tu.

Kufanikiwa au kuwa tajiri si kitu kibaya, kufanikiwa katika maisha ni kitu kizuri sana, na Mungu yupo tayari kukufanikisha, ila swali kubwa ni; Je utakapo fanikiwa sana hutamuacha Mungu? na kuona kwamba umefika hapo kwa nguvu zako?

Akawaambia watakapokula na kushiba wasimsahau. Leo watu wengi wamemsahau Mungu, wamesahau Mungu aliyewatoa katika shida na hali mbaya, sasa wapo kwenye raha hawakumbuki tena kuhusu Mungu. Wakati amabao huna chakula, huna pesa ulikuwa unalia mbele za Mungu, unaomba kwa bidii, lakini muda ambao chakula unacho tele, una pesa nyingi unapunguza kumpenda Mungu, unaanza kusema upo 'busy' sana mpaka kwenye siku yako huna muda wa kusoma Neno la Mungu na kuomba, baada ya kununua gari huwahi tena kanisani kama ulivyokuwa unatumia daladala. 

Unajua maisha yana vipindi vipindi, kuna kipindi cha kupungukiwa na kipindi cha kufanikiwa, sasa wakati unapitia kwenye shida huwa unamkumbuka Mungu lakini ukipata majibu yako unamsahau Mungu, acha hiyo tabia. Hayo mafanikio uliyonayo sio kwasababu ya nguvu zako bali ni Mungu aliyekutoa kwenye utumwa.

Kuwa na miradi mingi/ biashara sio mbaya lakini zisikufanye ukose muda wako na Mungu, ukose muda wa kwenda kanisani, kwenda katika ibada za katikati. Amua leo kubadilika na umkumbuke Mungu wako aliyekutoa katika siku zako za shida. Fauata sheria za Mungu na umtii Yeye.

No comments:

Post a Comment