''Badilisha Maisha yako kwa kumpokea Yesu Kristo kuwa Mwokozi wa Maisha Yako.''

Sunday, September 9, 2018

KIU NA NJAA YA NENO LA MUNGU

Mhubiri: Mch. Kiongozi, Abdiel M. Mhini
Maandiko: Zaburi 42:1-2

Sisi binadamu huwa tunapata njaa na kiu, na unapohisi njaa huwa unahitaji sana chakula ule ushibe bila hivyo hutaweza kutulia mpaka uitimize ile hamu ndani yako. Vivyo hivyo inapaswa tuwe na hamu kubwa ya kusoma Neno la Mungu, maana Neno ndio chakula cha roho yako. Usipokula chakula baada ya siku kadhaa nguvu itapungua na hatimaye utakufa; hali hiyo hiyo inatokea katika afya yako ya roho, ukiacha kusoma Neno kwa muda mrefu au unasoma Neno kidogo, roho yako inakuwa haina nguvu ya kumudu vita vya kiroho. 

Tatizo kubwa wakristo wengi wa siku za leo hawana muda mwingi wa kusoma Neno la Mungu. Ni lazima utenge muda maalum wa kusoma Neno la Mungu, kusoma Biblia iwepo kabisa kwenye ratiba yako. Na pia ujenge njaa na kiu ya Neno la Mungu. Mtu ambaye hana njaa hawezi kuhitaji kula sana bali mwenye njaa ndiyo anayekula sana. Jenga njaa ya kutaka  kulijua Neno la Mungu, hiyo itakufanya uweze kusoma sana Neno la Mungu.

Kama unataka uzidi kuwa karibu na Mungu ni lazima uwe msomaji mzuri wa Neno la Mungu. Kusoma Neno la Mungu kila siku ndiyo itakayokusaidia sana kukuwa kiroho. Kuacha kula chakula huko ni kufa, kuacha kusoma Neno kwa biddii ni kujitakia mwenyewe kifo cha kiroho. Badilika leo, kwenye ratiba yako tenga muda wa kusoma hata sura kadhaa za kwenye Biblia, nawe maisha yako yatabadilika, nguvu za kiroho zitaongezeka sana.

No comments:

Post a Comment