''Badilisha Maisha yako kwa kumpokea Yesu Kristo kuwa Mwokozi wa Maisha Yako.''

Tuesday, March 25, 2014

TAFUTA KUWA NA UWEPO WA MUNGU

UJUMBE: TAFUTA KUWA NA UWEPO WA MUNGU KWA GHARAMA YOYOTE KATIKA MAISHA YAKO. 
MHUBIRI: Mch. SANGA
Maandiko: 2Nyakati 5:2-14

Bila Uwepo wa Mungu kwenda pamoja na sisi, kwenda pamoja na kanisa tusingefika mahali popote. Uwepo wa Mungu ni wa maana sana kwa maisha ya kikristo. Maisha ya kikristo ni tofauti sana na maisha ya kidini, ukisoma kitabu cha Kutoka 33 yote, inaelezea Musa akitembea na Mungu, katika mstari wa 15, Musa alimwambia Mungu uso wako usipokwenda pamoja nami usituchukue kutoka hapa. Kwenda na Uwepo wa Mungu ni kitu cha muhimu sana, Musa alitambua hilo  na pia alitambua kuwa kizazi hiki kikiona Uwepo wa Mungu, Uwepo wa Mungu utaenda mpaka kizazi kingine. Uwepo wa Mungu ni zaidi ya vitu vinavyo onekana, watu wa dini kinacho kosekana ndani yao ni Uwepo wa Mungu.

Hakuna jukumu lililo la muhimu sana kama kubeba Uwepo wa Mungu ndani ya maisha yako. Kuwa mtu wa kubeba Uwepo wa Mungu katika maisha yako, adui hatafuti magari au vitu vyako lakini anatafuta kuondoa Uwepo wa Mungu ndani yako kwasababu anajua akikunyanganya Uwepo wa Mungu amekumaliza. Tunawajibu wa kubeba Uwepo wa Mungu kizazi mpaka kizazi. Uwepo wa Mungu ni kitambulisho cha Mungu uliye naye pia ni kitambulisho cha kanisa lililo hai. 

Ili Uwepo wa Mungu uonekane kuna mambo ya kufuata, tuna ahadi ya kutunza na kutembea na Uwepo wa Mungu. Kanuni tano(5) za kutembea na uwepo wa mungu. 

1. Ishi maisha ya Utakatifu, ishi maisha yanayofanana na ukristo ulinao, jitakase, wakristo wengi wanaishi tufauti na wanavyosema. Ishi kama Neno la Mungu linavyotaka uishi.

2. Jidhabihu, kujidhabihu ndio yawe maisha yako, jitoe mwenyewe kwa Mungu, je unamtafuta Mungu kwa muda gani?, je unakaa na Mungu kwa muda gani?, kizazi hiki watu wengi hawana muda wa kukaa katika Uwepo wa Bwana. Ndugu yangu kaa katika Uwepo wa Bwana, siku moja ya kukaa katika Uwepo wa Bwana ni zaidi ya miaka elfu moja ya kukaa bila Uwepo wa Bwana. Pia wafundishe watoto wako kukaa katika Uwepo wa Bwana. Mfalme Sulemani alichinja wanyama wengi kama sadaka kwa Mungu, na Mungu akashusha uwepo wake. Ndani ya Uwepo wa Mungu utaona kushinda zaidi ya kushinda. Tamani sana katika maisha yako uone Uwepo wa Mungu, Uwepo wa Mungu ni wa muhimu kuliko fedha na dhahabu, beba Uwepo wa Mungu zaidi kuliko fedha na dhahabu, Uwepo wa Mungu ni kitu cha maana sana. 

3. Ni lazima uwe na muda wa kumtumikia Mungu, na hicho ndicho kilichokosekana katika maisha ya leo. Ukimtumikia Mungu ndipo utakapo stawi, Uwepo wa Mungu hauji kwako kwa kuwekewa mikono na manabii wakubwa au wachungaji lazima umtumikie Mungu ili Mungu aone huyu mtu anafaa ili akuzidishie Uwepo wake. 

4. Lazima uwe mtu wa kutunza maagano, lazima utunze maagano ya Mungu, lazima utunze mapenzi ya Mungu, Paulo alisema uwe mtu wa kutunza maungamo yako, Tunza mapatano yako yale uliyokubaliana na Mungu, Hicho ndicho kilichomfanya Mungu atembee na Ibrahimu, na Musa, simama katika patano lako na Mungu aliye hai

5.Lazima uwe mtii katika yale mapatano ya Mungu sawa sawa na Neno la Mungu, heshimu na kutenda lile Mungu alilokuagiza kutenda.

Hasara ya kuto kuwepo na uwepo wa Mungu ni mbaya sana, muangalie Eli alikuwa ni mtumishi wa Mungu aliposikia sanduku la agano limechukuliwa Eli akafa pale pale kwasababu alijua Uwepo wa Mungu umeondoka Israel.  bila Uwepo wa Mungu Israel ilikuwa ipo kwenye hatari kubwa sana ya kupigwa, na muda mwingine wana wa Israel walikuwa na sanduku la Bwana lakini walikuwa wanapigwa kwasababu walikuwa hawafuati kanuni za Mungu, hawa ni sawa na wakristo vuguvugu. Kuwa makini, shetani anatafuta kuondoa Uwepo wa Mungu katika maisha yako, tamani Uwepo wa Mungu uende nawe, tafuta kwa gharama zozote kujaa na Uwepo wa Mungu maadui hawatakupiga, tafuta kutunza uwepo wa Mungu kwa gharama yoyote. Kama Uwepo wa Mungu ukiondoka kwako hautaweza kufanya kitu chochote. Leo ndugu yangu unahitaji kutafuta Uwepo wa Mungu na kukaa katika Uwepo wa Mungu. Lazima ubaki katika Uwepo wa Mungu.

Mchungaji Sanga akiwa anahubiri

No comments:

Post a Comment