Mhubiri : Rev. Ezekiah Mwakajwanga
Maandiko: Mathayo 25:1-12
Yesu yu karibu, anarudi upesi.
kabla hajaenda msalabani Bwana Yesu alitoa usia mwingi juu ya kurudi kwake. Alisisitiza sana tumtafute kwa bidii, Bwana Yesu yupo na yule amtafutaye kwa bidii na huyo afanyae hivyo atamuona.
Kurudi mara ya pili kwa Bwana Yesu ni jambo ambalo linaugusa ulimwengu mzima lakini linatuhusu sana wana wa Mungu tuliokoka. Katika Mathayo 24:3 na kuendelea inaelezea wanafunzi wa Yesu walipomfuata Yesu kwa faragha na kumuuliza kwa habari ya siku za mwisho, kwenye sura inayofwatia Mathayo 25, Yesu akawajibu kwa mfano wa sherehe ya harusi.
Katika huu mfano tunafunuliwa vidokezo muhimu vifwatavyo:
- Wote walikuwa ni wanawali.
- Wanawali wote hawa walipaswa kuweka nuru kwa kutumia koroboi itumiayo mafuta.
- Wanawali wote wakawasha koroboi zao na kumsubiri bwana harusi.
- Wanawali wote walikuwa wanafanana katika mambo yote KAMA WANAWALI lakini nusu yao walikuwa na siri, walikuwa na akili na wengine walikuwa ni wapumbavu.
Katika wakati wa sasa kuna watu wengi walio makanisani wanaoigiza mambo ya kiroho, kama wale wanawali wapumbavu waliomsubiri bwana harusi bila mafuta ya kutosha. Na mafuta yao yalipoisha, wakatoka kuongeza mafuta, punde Bwana Harusi akafika na kufunga mlango ikawa hasara kwa wanawali wale waliotoka kwenda kununua mafuta. Na waliporudi Bwana harusi akawaambia siwajui ninyi, ndivyo itakavyokuwa kwa mtu anayeigiza mambo ya kiroho mwenye wokovu wa jina tu na matendo yake ni kinyume na wokovu wake.
Katika wakati wa sasa watu wote wanaoigiza mambo ya kiroho mafuta yao yamekwisha maana dhambi imewatawala, na Roho Mtakatifu ambaye ndiyo hayo mafuta ameondoka. Bwana harusi Yesu Kristo atakavyokuja atawaambia siwajui ninyi.
Jaza mafuta sasa ili Bwana harusi akirudi akukute upo tayari. Mafuta ni Roho Mtakatifu, Roho Mtakatifu / mafuta ni wa mihimu sana, bila Roho Mtakatifu hutaweza kuangaza wewe na bila Roho Mtakatifu hutaweza kupata nguvu ya kuishinda dhambi.
No comments:
Post a Comment