Mhubiri: Mch. Kiongozi Abdiel M. Mhini
Maandiko: 2Petro 3:1-4
2Petro 3:1-4
"Wapenzi, waraka huu ndio wa pili niwaandikiao ninyi; katika zote mbili naziamsha nia zenu safi kwa kuwakumbusha, 2 mpate kuyakumbuka yale maneno yaliyonenwa zamani na manabii watakatifu, na ile amri ya Bwana na Mwokozi iliyoletwa na mitume wenu. 3 Mkijua kwanza neno hili ya kwamba katika siku za mwisho watakuja na dhihaka zao watu wenye kudhihaki, wafuatao tamaa zao wenyewe, 4 na kusema, Iko wapi ahadi ile ya kuja kwake? Kwa maana, tangu hapo babu zetu walipolala, vitu vyote vinakaa hali iyo hiyo, tangu mwanzo wa kuumbwa."
1Yohana 2:18 "Watoto, ni wakati wa mwisho; na kama vile mlivyosikia kwamba mpinga Kristo yuaja, hata sasa wapinga Kristo wengi wamekwisha kuwapo. Kwa sababu hiyo twajua ya kuwa ni wakati wa mwisho."
Biblia inaweza wazi kuhusu majira na nyakati za siku za mwisho, lakini je ni kwa kiasi gani unatambua kwamba hizi ni siku za mwisho? yakupasa uelewe kwamba majira haya tuliyonayo ni ya siku za mwisho, na kila dalili inaonyesha wazi kuwa hizi ni siku za mwisho. Wapinga kristo sasa wamekuwa ni wengi tena wapo wazi wazi, wameshikilia ndoa za jinsia moja ambayo ni kinyume kabisa na mapenzi ya Mungu.
Je baada ya kujua kwamba tupo kwenye siku za mwisho unafanyaje?
Petro alikuwa analikumbusha kanisa kwamba wawe makini katika siku hizi za mwisho. hizi siku za mwisho ni za kuwa makini sana na kujiepusha na mitago ya shetani ya kila namna ili usije ukaachwa.
2Timotheo 3:1-5
"Lakini ufahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari. Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi, wasiowapenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema, wasaliti, wakaidi, wenye kujivuna, wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu; wenye mfano wa utauwa, lakini wakikana nguvu zake; hao nao ujiepushe nao."
Paulo pia alimkumbusha Timotheo kuhusu hizi siku za mwisho, kwamba awe makini na siku za mwisho. Dalili zote za siku za mwisho zilizoandikwa hapo juu zimetimia. Siku za leo watu wanapenda sana hela kuliko kawaida watu, hawajali utu wa watu wanaangalia tu hela, hela kwanza hata mambo ya Mungu wanaona yanawachelewesha wanataka wakatafute hela, wakienda kanisani wanataka sana uwaombee wapate hela sio roho zao zimpate Yesu. Watu wamekuwa wavivu sana kuja ibada za katikati, watu hawaji kwenye mkesha. Watu wamekuja wenye kujivuna wasio penda kutenda mema. Sasa utambue kwamba majira yamefika rekebisha maisha yako na Yesu.
Nyakati hizi za mwisho wamekuja manabii wa uongo wengi, makanisa mapya yamekuja mengi kila mtu anasema lake mara huyu anasema chumvi huyu mafuta, usidanganyike mpendwa kuwa makini sana sana, haya yote yalitabiriwa kuwa yatatokea na sasa ndo yameanza kutokea kwahiyo kuwa makini usidanganywe, usidanganyike! Jina la Yesu linajitosheleza hakuna haja ya mafuta wala chumvi! Mkabidhi Yesu maisha yako ayabadilishe na vifungo vyote vitakuacha, hauhitaji chumvi wala mafuta wala kutoa hela ili uombewe!
Vitu Muhimu vya kufanya nyakati hizi za siku za mwisho
1. Usiipende dunia, acha kabisa kuipenda dunia na mambo yake kama taama za mwili, tamaa za macho na kiburi cha uzima. 1Yohana 2:15-17
2. Kuwa na uhusiano mzuri na Mungu, Soma Neno la Mungu kila siku! omba kwa bidii na msikilize Roho Mtakatifu
3. Ishi kwa tahadhari kusubiri kurudi kwa Yesu
4. Watambue manabii wa uongo, kipindi cha sasa ni wengi mno, wanaweza kuonekana kwamba ni watumishi waliofanikiwa sana na kutenda miujiza sana lakini ni wa uongo, tulia kwa Yesu.
5. Ipende Kweli ya Yesu 1Yohana 4:1-4
No comments:
Post a Comment