''Badilisha Maisha yako kwa kumpokea Yesu Kristo kuwa Mwokozi wa Maisha Yako.''

Sunday, December 4, 2016

TEMBEA NA ROHO MTAKATIFU, ILI UWE NA MAISHA YA USHINDI

Mhubiri: Mch. Enock, Kigamboni
Maandiko: Matendo 13:1-3, 4-12, 13
 
Matendo 13:1-3
"1 Na huko Antiokia katika kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa ndugu wa kunyonya wa mfalme Herode, na Sauli. 2 Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia. 3 Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao."
 
Hapa tunaona kuchaguliwa kwa Barnaba na Sauli. Baada ya kanisa la Antiokia kuwa na ibada nzuri tena ya kufunga na kuomba ndipo Roho Mtakatifu akashuka na kuwachagua Barbana na Sauli. Roho Mtakatifu anashuka katika mazingira matakatifu, watu wakijitakasa na kumkaribia Mungu Roho Mtakatifu huwa anashuka na kuhudumia watu,kutoa majibu ya mahitaji ya watu. Roho Mtakatifu akishuka atakufunulia jambo la kufanya na kujibu mahitaji yako, yakupasa tu kuwa msafi na mtakatifu maana Roho Mtakatifu hashuki sehemu iliyo chafu.
 
Baada ya Roho Mtakatifu ndipo kazi inapoanza au huduma inapoanza, ndio maana (Matendo 1:4 "Hata alipokuwa amekutana nao aliwaagiza wasitoke Yerusalemu, bali waingoje ahadi ya Baba, ambayo mlisikia habari zake kwangu") Yesu aliwaambia wanafunzi wake wasitoke Yerusalemu mpaka watakapo pokea Nguvu, na tunaona katika Matendo 2 katika siku ya Pentekoste wakapokea ile Nguvu ya Roho na kuanza kazi rasmi ya kumtangaza Yesu kwa ujasiri na huduma nyingine nyingi zikaanza hapo.
 
Kila mmoja kuna kazi uliyoitiwa, kazi maalum kwa ajili ya kujenga ufalme wa Mungu, ili uijue kazi yako ni lazima uwe na Roho Mtakatifu ndani yako ili akuonyeshe ni wapi sehemu yako, na ili ufanikiwe katika maisha yako ya kiroho na ya kimwili pia ni lazima ukae PALE ULIPOITIWA na sio kukaa kila eneo au kujaribu kufanya kila huduma bali una huduma yako maalum uliyopewa ukiifanyia kazi hiyo kwa bidii ndipo utakapo fanikiwa sana.
 
Pasipo Roho Mtakatifu utapotea maana Yeye tu ndiye msaidizi tuliyeachiwa na Yesu lakini wakati huo huo Yeye pia ni nafsi ya Mungu, kwahiyo ndiye anayejua wapi ufanye kitu gani kwa wakati upi. Huduma za watu wengi baada ya muda huwa zinakufa kwasababu ya kuacha kumsikiliza Roho Mtakatifu, ukijiongoza mwenyewe na kutegemea akili zako ni hakika kabisa huduma yako itakufa.

No comments:

Post a Comment